Jitokezeni uzinduzi Mbio za Mwenge

0
276

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi amesema Mbio za Mwenge wa Uhuru zitazinduliwa Aprili 2, 2024 na hivyo amewataka Watanzania wajitokeze kwa wingi kwenye uzinduzi huo utakaofanyika katika Mkoa wa Kilimanjaro.

Amesema hadi sasa maandalizi ya uzinduzi wa mbio hizo yamefikia zaidi ya asilimia 90 hivyo amehimiza Mkoa wa Kilimanjaro kuhahamasisha kadri wawezavyo wananchi kushiriki kwa wingi katika tukio hilo.

Katambi ameyasema hayo wakati akikagua maandalizi ya uzinduzi wa Mbio za Mwenge katika Uwanja wa Michezo wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU), Mkoani Kilimanjaro.

Amesema Mbio hizo za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka huu 2024 zinaadhimisha miaka 60 tangu zianzishwe rasmi mwaka 1964, zikienda sambamba na miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.

Katambi ameupongeza mkoa huo kwa utayari na maandalizi mazuri yanayoendelea. Mbio za mwaka huu 2024 zinaogozwa na kaulimbiu isemayo “Tunza Mazingira na Shiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Ujenzi wa Taifa Endelevu.”