Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Geophrey Pinda amewataka wananchi wa Wilaya ya Mbulu mkoani Manyara kujitokeza kwa wingi kuomba maeneo yao ya ardhi yatambuliwe.
‘’Naomba mwendelee kujitokeza kwa wingi ili maeneo yenu yatambuliwe na hii itasaidia sana wanachi wa Mbulu kutogombana katika masuala ya ardhi kwa kuwa kila mmoja atakuwa na hati yake,’’ amesema Pinda.
Ametoa kauli hiyo akiwa katika Halmashauri ya Mji wa Mbulu wakati wa zoezi la kutoa hati kwa wananchi waliotambuliwa kupitia mradi wa Kupanga, Kupima na Kumilikisha (KKK).
Jumla ya wamiliki wa ardhi 68 katika Wilaya ya Mbulu walikabidhiwa hati miliki za ardhi zilizopatikana kupitia mradi huo wa KKK.