Jitoeni kwa ajili ya wengine

0
328

Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa Watanzania kutumia Sikukuu ya Pasaka kutambua kwamba hakuna ushindi bila kujitoa muhanga kwa ajili ya wengine, familia, wahitaji na Taifa kwa ujumla.

Dkt. Mpango ametoa wito huo leo Machi 31, 2024 alipotoa salamu za Sikukuu ya Pasaka mara baada ya kushiriki na waumini mbalimbali Ibada ya Sikukuu ya Pasaka katika Kanisa Katoliki, Parokia ya Bikira Maria, Mama wa Damu Azizi ya Yesu – Kisasa mkoani Dodoma.

Amesema ni lazima kujitoa muhanga kwa kutimiza wajibu vizuri, kwa kufanya kazi kwa bidii kwa ajili ya maendeleo ya nchi, sasa na kwa vizazi vijavyo.

Makamu wa Rais amesema ni muhimu kutumia Sikukuu ya Pasaka kujifunza kushinda ubinafsi na kuhakikisha haki na huduma zinatolewa bila kuomba rushwa.

Dkt. Mpango ametoa wito kwa viongozi na watumishi wa serikali kuwa kielelezo cha kujitoa muhanga kwa ajili ya kuwatumikia watu wengine. Amesema Watanzania wanapaswa kuendelea kumcha Mungu pamoja na kutunza urithi wa dunia uliyotolewa na Mwenyezi Mungu ikiwemo mazingira.

Ibada hiyo ambayo Dkt. Mpango aliongozana na mwenza wake, Mama Mbonimpaye Mpango, imeongozwa na Padre Vedastus Ngowi kwa kushirikiana na Paroko wa Parokia hiyo, Sostenes Ndendya.