Jiji la Arusha laadhimisha siku ya Usonji

0
470

Shirika la Connects Autism Tanzania linalotoa huduma kwa watu wenye Usonji, limeipongeza serikali kwa kutoa huduma ya wataalamu, chakula, vifaa na ile ya afya kwenye vitengo vinavyohudumia watoto wenye Usonji.

Pongezi hizo zimetolewa na Mkurugenzi wa Shirika hilo Graceanna Lyimo wakati wa maadhimisho ya siku ya Usonji katika halmashauri ya jiji la Arusha.

Lyimo amesema kuwa changamoto kubwa iliyopo sasa ni upungufu wa walimu wanaofundisha watoto wenye Usonji, jambo linalokwamisha watoto wenye tatizo hilo kupata elimu sahihi na kwa wakati.

Afisa Elimu Msingi katika halmashauri ya jiji la Arusha, -Omary Kwesiga ndiye alikua mgeni rasmi wakati wa maadhimisho hayo ya siku ya Usonji kwa halmashauri ya jiji la Arusha na amewataka wazazi wote kuhakikisha watoto wenye Usonji wanapata elimu kwa wakati.

Wakizungumzia siku hiyo ya Usonji, baadhi ya wazazi katika halmashauri ya jiji la Arusha wamesema kuwa, tabia ya baadhi wazazi wa kiume kuwaachia kazi ya ulezi wazazi wa kike pindi wanapobaini mtoto kuwa na Usonji, inasababisha watoto wenye tatizo hilo kukosa huduma muhimu ikiwemo elimu.