JICA watembelea ofisi za TBC

0
208

Uongozi wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA) umetembelea ofisi za Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) zilizopo Mikocheni mkoani Dar es Salaam na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo Dkt. Ayub Rioba Chacha.

JICA ambayo inaadhimisha miaka 60 ya ushirikiano wake na Tanzania inakusudia kufanya kongamano la ubunifu (The Japan-Tanzania Innovation Forum) kwa siku mbili katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambapo kwa siku ya kwanza litaongozwa na Dkt. Rioba.

Kongamano hilo litahusisha wadau 300 kutoka ndani na nje ya nchi, ikiwa ni pamoja na viongozi wanaohusika na sekta ya elimu, sayansi na teknolojia, mipango ya maendeleo, mazingira, viwanda na uwekezaji pamoja  na wafanyabiashara, waandishi wa habari na wanafunzi kutoka Tanzania, Japan na mataifa mengine.

Katika siku mbili za kongamano hilo (Februari 9 na 10, 2023) washiriki watajadili mambo mbalimbali ya teknolojia na ubunifu kwa kuangazia mambo ambayo Tanzania inaweza kujifunza kutoka Japan kwenye sekta hiyo, vikwazo vinavyoikabili Tanzania katika kukuza sekta ya teknolojia na ubunifu na namna bora ya kuimarisha ushirikiano kati ya Japan na Tanzania kupitia ubunifu.