Jeshi la Polisi nchini limesema kuwa ni kweli Mussa Sadick mkazi wa mkoani Tabora alibambikiziwa kesi ya mauaji na kwamba tayari jeshi hilo lilikuwa limeshapata barua ya malalamiko ya mwanachi huyo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam, Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini Ahmed Msangi amesema kuwa baada ya kupata barua hiyo jeshi hilo lilituma afisa wake kwenda mkoani humo kushughulikia suala hilo na baada ya kufika kule aligundua ukiukwaji wa taratibu za kisheria.
Msangi amesisitiza kuwa hatua stahiki zitachukuliwa kwa watu wote waliokiuka sheria na kusababisha jambo hilo pindi uchunguzi utakapokamilika.
Jeshi la polisi nchini limetoa kauli hiyo ikiwa ni siku moja tu baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Biswalo Mganga kumwondolea mamlaka askari polisi aliyejulikana kwa jina la Tengwa ya kuendesha kesi za jinai kutokana na kukiuka haki na uonevu aliofanyiwa mkazi huyo wa Tabora,- Mussa Sadick kubambikiziwa kesi ya mauaji huku kesi ya msingi ikiwa ni kosa la unyang’anyi.
Biswalo alichukua hatua hiyo baada ya Rais John Magufuli kusoma barua ya mlalamikaji katika chombo kimoja cha habari juu ya kubambikiziwa kesi ya mauaji.
Tarehe Nane mwezi huu, Sadick alimwandikia barua Rais Magufuli kuhusu kubambikiziwa kesi ya mauaji namba 8/2018 katika Mahakama ya Tabora baada ya kuwekwa ndani kwa muda wa wiki moja kwa kosa la unyang’anyi.
Tayari Sadick ameachiliwa huru.