Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa amesema kuwa Jengo la Abiria katika Uwanja wa Ndege wa Songwe litakamilika na kuanza kutumika mwishoni mwa mwezi huu.
Waziri Prof. Mbarawa ametoa kauli hiyo baada ya kukagua maendeleo ya mradi wa jengo hilo na kuridhishwa na hatua ya ujenzi wake ambao kwa sasa umefikia asilimia 98.
Ameitaka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) kuhakikisha jengo hilo linatoa huduma za viwango kwa kuzingatia taratibu za kimataifa zinazoongoza usafiri wa anga.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Juma Homera amesema kukamilika kwa jengo hilo kutakifanya Kiwanja hicho kuwa na hadhi ya Kimataifa kwani kitawapunguzia usumbufu abiria hasa zinapokuja ndege kubwa.