Jela maisha kwa kulawiti mtoto mdogo

0
152

Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoani Tabora imemhukumu kijana, Benard Meshack (26) kifungo cha maisha jela baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kumfanyia ukatili wa kijinsia mtoto mwenye umri wa miaka minne.

Adhabu hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Jovin Kato baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo juu ya tuhuma zilizokuwa zikimkabili kijana huyo za kufanya mapenzi kunyume cha maumbile na mtoto mdogo ambaye jina lake limehifadhiwa.

Akisoma hukumu hiyo Hakimu Kato amesema, baada ya mahakama kusikiliza maelezo ya pande zote mbili imeridhika pasipo shaka kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo la kinyama na kubainisha kuwa adhabu inayostahili kwa kosa hilo ni kifungo cha maisha.

Awali upande wa mashitaka ukiongozwa na wakili Tito Mwakalinga umeieleza mahakama kuwa, mshitakiwa alitenda kosa hilo Julai 02, 2020 alipokuwa amemfuata mtoto huyo shuleni ili kumrudisha nyumbani.

Wakili Mwakalinga ameongeza kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo kinyume na kifungu namba 154 (1) (a) na (2) cha sheria ya makosa ya jinai Sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2019.