Jamii yatakiwa kuwasaidia wenye uhitaji

0
1583

Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Tulia Ackson ametoa wito kwa jamii nchini kuendelea kusaidia watu wenye mahitaji maalumu.

Dkt Tulia ametoa wito katika ofisi za Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) eneo la Mikocheni jijini Dar es salaam, alipofika kwa lengo la kukabidhi msaada wa viti mwendo viwili, pesa taslimu zaidi ya Shilingi Milioni Sita, kitanda na godoro  kwa mtoto Amos Gabriel mkazi wa jiji la Mbeya aliyeanguka kutoka juu ya mti na  kuvunjika uti wa mgongo.

Pia amewashukuru watu wote waliojitokeza na kumsaidia mtoto Amos na kuwataka Watanzania wote wenye mapenzi mema kujitokeza na kuwasaidia wenye uhitaji.

Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Tulia Ackson  ndiye aliyemsafirisha Mtoto Amos kutoka jijini Mbeya kwenda jijini  Dar es salaam kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

Tukio la kuanguka kwa mtoto Amos lilitangazwa na TBC kupitia kipindi chake cha  televisheni cha  Wape Nafasi na hivyo kusababisha wadau mbalimbali kujitokeza na kumpatia msaada.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania Dkt Ayub Rioba amewashukuru Watanzania kwa ukarimu waliouonyesha katika kumsaidia mtoto Amos na wengine wanaohitaji misaada ya aina mbalimbali.

Amos mwenyewe amewashukuru watu wote waliompatia msaada na kuwashauri watu wenye ulemavu kutokana tamaa, bali wafanye bidii ili kutimiza ndoto zao.

Mtoto Amos mwenye umri wa miaka Kumi na Minne  alivunjika uti wa mgongo baada ya kuanguka kutoka juu ya mti  alipotumwa kukata fimbo akiwa shuleni mwezi wa Aprili mwaka huu.