Jamii yatakiwa kutofumbia macho wanaotweza utu wa mwanamke

0
212

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imeitaka jamii kuendelea kubeba jukumu la kutokuyafumbia macho matukio yote yenye kutweza utu wa mwanamke na kutoa taarifa katika mamlaka husika pindi wanaposhuhudia matukio hayo.

Hayo yalibainishwa na Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Jaji Mstaafu, Mathew Mwaimu katika taarifa yake kwa vyombo vya habari ya kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani (Machi 8, 2021).

“Kupitia jitihada mbalimbali za uhamasishaji zilizofanyika nchini kumekuwepo na ushiriki wa wanawake katika masuala ya uongozi kwenye vyama vya siasa, serikali, bunge, mahakama na katika nafasi nyingine za uongozi katika jamii,’” amesema Jaji Mwaimu.

Aliongeza kuwa pamoja na jitihada mbalimbali za Serikali za kukemea vitendo vya ukatili kwa wanawake bado kumekuwepo na changamoto mbalimbali zinazowakabili wanawake katika kuwania nafasi za uongozi zikiwemo mila na desturi zinazominya haki za wanawake, elimu na kipato duni kwa wanawake wenye nia ya kugombea uongozi na kutojiamini.

“Tume kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imekuwa ikiwahimiza wanawake kuendelea kujitokeza kuwania nafasi mbalimbali za uongozi kuanzia ngazi za kijiji/mtaa hadi taifa na kuwajengea uwezo wa namna ya kudai haki zao kisheria pale wanapohisi haki hizo kuvunjwa,” amefafanua Mwaimu

Kaulimbiu ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani mwaka huu 2021 ni ‘Wanawake Katika Uongozi: Chachu kufikia Dunia Yenye Usawa.’