Jamii ielimishwe tafsiri ya neno nasaha

0
213

Mhadhiri Msaidizi kutoka Idara ya Saikolojia na Unasihi Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) George Mwala amesema ipo dhana kwamba mtu anapohitaji nasaha kutoka kwa Mnasihi ana maambukizi ya virusi vya Ukimwi.Amesema hali hiyo husababisha wasio na changamoto hiyo kukosa huduma ya unasihi kwa kushindwa kujitokeza ili wasaidike wanapokuwa na changamoto tofauti na hiyo.George amesema yapo masuala yanayowakumba wanafunzi shuleni ambayo yanahitaji huduma ya unasihi akiyataja kuwa ni pamoja na uchaguzi wa masomo wakati wa kuchagua Tahasusi, maandalizi ya masomo yanayoelekea kubeba hatima zao, changamoto za kisaikolojia, mahusiano ya wanafunzi na jamii inayowazunguka na maendeleo ya kielimu.Akitoa mafunzo kwa walimu wa sekondari juu ya mada inayohusu maeneo ya ushauri, unasihi na malezi mkoani Lindi wakati wa semina ya programu ya mpango wa Shule Salama iliyopo chini mradi wa kuimarisha Ubora wa Elimu ya Sekondari (SEQUIP) George ameongeza kuwa ni vema kwa Mnasihi kujitambulisha kwanza na kutoa ufafanuzi kuhusu tafsiri halisi ya unasihi kusudi wanafunzi wapate uelewa sahihi wa huduma hiyo ili waweze kusaidika.Aidha. amesema wapo wanafunzi ambao hata baada ya kuelimishwa dhana ya unasihi huwa waoga kufuata huduma hiyo, hivyo ni vema walimu hao wakawajengea mazingira rafiki hata kwa kutumia mbinu ya unasihi rika ambayo inampa nafasi mwanafunzi kumuagiza mwanafunzi mwenzake kumtengenezea njia ya kupata huduma hiyo kutoka kwa mwalimu husika.