Jaji Mutungi avitaka vyama vya siasa kuheshimu sheria na taratibu za uchaguzi

0
445


Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi amewataka viongozi wa vyama vya siasa na wadau wote kuheshimu sheria na taratibu za Uchaguzi kama zilivyoainishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ili kuepuka migogoro isiyo ya lazima.

Akizungumza Jijini Dar es Salaam,  katika kikao kati ya viongozi wa vyama vya siasa amesema “hiki si kikao cha kuja kusutana ila ni kikao cha kuja kuongea na kuangalia mwelekeo unavyokwenda kwenye kampeni, lakini pia nafasi ya Msajili kama mlezi nikaona nisiwanyime hiyo nafasi ya kukutana nanyi na kuwapa maneno mawili ya kuwakumbusha wajibu wenu.”

 Jaji Mutungi amewaomba wagombea pamoja na wadau wa vyama vya siasa kuimarisha Demokrasia ya nchi kwa kufanya siasa za kistaarabu ambapo amewataka wagombea washindane kwa ustaarabu huku wakifuata sheria na taratibu za nchi.

 Aidha ameeleza kuwa mtu yoyote atakayeonekana kwenda kinyume na maelekezo na taratibu za Uchaguzi atachukuliwa hatua kulingana na taratibu zilizowekwaza uchaguzi Mkuu 2020

“Tuachane na ile dhana ya kwamba mtu anasema wakiniacha wananiogopa, wakinishughulikia wananionea, sasa huu ujumbe ninaousema uende pande zote, na sisi taasisi ambazo zimepewa mamlaka ya kusimamia utekelezaji wa hii sheria, tuisimamie kwa haki kwa sababu tusipofanya hivyo tunaweza sababisha tafarani” amesisitiza.