Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Selemani Jafo ameeleza kuridhishwa na uzingatiaji wa sheria ya mazingira katika utekelezaji wa mradi wa bwawa la kufua umeme wa maji la Julius Nyerere (JNHPP) kwenye bonde la mto Rufiji
Waziri Jafo amesema hayo mara baada kufanya ziara ya kikazi ya kukagua uzingatiaji wa masharti yaliyowekwa katika Cheti cha Tathmini ya Athari kwa mazingira kinachotolewa na ofisi yake.
Amesema ameridhishwa na maelezo yaliyotolewa na Mhandisi Mkazi wa TEKU John Mageni, kuhusu hatma ya mashimo yanayochimbwa kwa ajili ya upatikanaji wa madini ujenzi ikiwemo mawe, kokoto na mchanga.
“Nimeridhika na maelezo ya wataalam wetu kuwa mashimo haya yatatumika kama chanzo cha mazalia ya viumbe hai wa majini baada ya mradi kukamilika, nimefarijika sana.” amesisitiza Jafo
Amemuagiza Mhandisi Mkazi na Wakandarasi katika mradi huo kuhakikisha kuwa vyuma chakavu na taka za kielektroniki zinazozalishwa katika mradi huo zinafuata taratibu za kimazingira na kuuzwa kwa Wafashabiashara wenye vibali vya Serikali vya mazingira.
Akikagua mfumo wa Maji taka katika eneo la ujenzi, Waziri Jafo ameagiza Afisa Mazingira wa mradi huo kuhakikisha anatunza takwimu za kiasi cha maji taka yanayozalishwa katika eneo hilo.
Ujenzi huo wa bwawa la kufua umeme la Mwalimu Nyerere umefikia asilimia 54 ya utekelezaji kati ya asilimia 59 zilizokusudiwa na unaratajiwa kukamilika mwezi June mwaka 2022.