Ijue Siku ya Wanawake Duniani

0
337

Siku ya Kimataifa ya Wanawake Duniani (IWD) ni sikukuu ambayo nchi nyingi zimekuwa zikiiadhimisha kila mwaka ifikapo Machi 8 na sasa maadhimisho haya yamedumu kwa zaidi ya karne moja.

Kila mwaka, maadhimisho huwa na mada maalumu ambapo kwa mujibu wa Tovuti ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake mwaka huu mada iliyochaguliwa ni “Kuhamasisha Ushirikishwaji” inayolenga kuhakikisha waandaaji na matukio yanajielekeza katika kuvunja vikwazo, kupinga dhana potofu, na kuunda mazingira ambapo wanawake wote wanathaminiwa na kuheshimiwa.

Kaulimbiuu ya Umoja wa Mataifa kwa mwaka huu wa 2024 ni “Wekeza kwa wanawake: Ongeza kasi ya maendeleo.” Ni siku ya kutathmini hali ya wanawake, kusherehekea mafanikio yao na kuendelea kupigania usawa wa kijinsia.

Siku hii ilitokana na harakati za wafanyakazi jijini New York, Marekani mwaka 1908, wakati wanawake 15,000 walipoandamana kudai haki ya kupata muda mfupi wa kufanya kazi, malipo bora na haki ya kupiga kura.

Mwaka 1910 mwanaharakati wa kikomunisti na mtetezi wa haki za wanawake, Clara Zetkin alirejelea tukio la New York kwenye Mkutano wa Kimataifa wa Wanawake Wanaofanyakazi huko Copenhagen, Denmark na pendekezo lake la kuwa na siku ya wanawake kimataifa liliungwa mkono kwa kauli moja na wanawake 100 kutoka nchi 17 waliohudhuria mkutano huo.

Siku ya kwanza ya Kimataifa ya Wanawake iliadhimishwa mwaka 1911 katika nchi za Austria, Denmark, Ujerumani na Uswizi.
Siku iliadhimishwa kwa mara ya kwanza na Umoja wa Mataifa mwaka 1975.

Imeandikwa na (Happyness Hans)