IGP Wambura apangua makamanda wa mikoa

0
191

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Camillus Wambura amefanya mabadiliko ya makamanda wa polisi wa mikoa katika kuboresha na kuongeza ufanisi wa utendaji kwenye mikoa mitatu.

Taarifa iliyotolewa leo Ijumaa Januari 06, 2023 na Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime imeeleza kuwa katika mabadiliko hayo, IGP Wambura amemhamisha aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Fortunatus Muslim kwenda Kitengo cha Mipango Makao Makuu ya Polisi Dodoma na nafasi yake ikichukuliwa na Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Alex Mukama ambaye alikuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe.

IGP Wambura amemhamisha Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Theopista Mallya kwenda kuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe.

Aidha, amemhamisha Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Shadrack Masija ambaye alikuwa Afisa Mnadhimu Namba Moja Mkoa wa Simiyu kwenda kuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa.