Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Simon Sirro amewahakikishia Watanzania kuwa hali ya usalama nchini na nchi jirani ya Rwanda ni salama.
IGP Sirro amesema hali ni salama kutokana na makubaliano kati ya Tanzania na Rwanda kufuatia operesheni za pamoja katika kushughulikia uhalifu unaovuka mipaka, matishio ya ugaidi na matishio mengine ikiwemo usafirishaji wa binadamu na biashara ya dawa za kulevya.
Mkuu huyo wa Jeshi la Polisi nchini ameyasema hayo mkoani Dar es salaam alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Jeshi la Polisi la Rwanda Kamishna Jenerali Dan Munyuza ambaye yupo nchini kwa ziara ya kikazi.
Katika mazungumzo yao viongozi hao wamekubaliana kuendelea kushirikiana na kubadilishana taarifa za wahalifu pamoja na kushughulikia uhalifu bila kuwa na vikwazo vya mipaka, ili kuwahakikishia maendeleo ya kiuchumi Wananchi wa pande zote mbili.
Kuhusu watu wanaoenda kujiunga na makundi ya uhalifu nchini Msumbiji, IGP Sirro amesema wamekubaliana kuweka mkakati utakaowezesha kuwapata wahusika pamoja na watu wanaofadhili makundi hayo ya uhalifu ili sheria ichukue mkondo wake.
Kwa upande wake Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Rwanda, Kamishna Jenerali Dan Munyuza amesema wamekubaliana na IGP Sirro kukutana mara kwa mara na kufanya mafunzo ya pamoja na kutekeleza makubaliana waliyoyafikia katika kukomesha matishio ya kigaidi na uhalifu mwingine ukiwemo ule unaovuka mipaka.