Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, -Kangi Lugola ameitaka Idara ya Uhamiaji Nchini kutokuwa kikwazo kwa Wawekezaji kutoka nje wanaotaka kuwekeza nchini kwa kutowabughudhi na badala yake wawaelekeze ili wafuate sheria za nchi.
Waziri Lugola ameyasema hayo mjini Moshi mkoani Kilimanjaro wakati akifungua kikao kazi cha Maafisa Waandamizi wa Idara ya Uhamiaji Nchini.
Waziri Lugola amesema kuwa, amelazimika kutoa kauli hiyo kutokana na kuwepo kwa taarifa kwamba, kuna baadhi ya Maafisa Uhamiaji wamekua wakiwabugudhi Wawekezaji kutoka nje, jambo ambalo ni hatari kwa nchi.
Amesema kuwa amekua akipokea malalamiko kama hayo kutoka kwa baadhi ya Wawekezaji, hivyo ni vyema Maafisa Uhamiaji wanaohusika na vitendo hivyo kuacha mara moja.
Waziri Lugola amesisitiza kuwa dhamira ya serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Magufuli ni kuhakikishia kuna mazingira mazuri kwa ajili ya Wawekezaji pamoja usalama wao na mali zao pindi wawapo nchini.