Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma amesema kuwa licha ya idara ya mahakama nchini kuendelea kufanya kazi nzuri bado inakabiliwa na upungufu wa watumishi.
Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya sheria nchini ikiwa ni mwanzo wa kuanza kwa shughuli za mahakama, Jaji Mkuu amesema kuwa mahitaji ya idara hiyo ni watumishi 10, 351 lakini waliopo sasa ni 5, 947 tu.
Jaji Mkuu ameongeza kuwa idadi ya watumishi wa mahakama imekua ikiendelea kupungua mwaka hadi hadi mwaka, ambapo kuanzia mwezi Januari hadi Disemba mwaka 2019 watumishi 258 waliondoka kazini kwa sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kustaafu, kuhama na vifo.
Kufuatia hali hiyo, Jaji Mkuu Profesa Ibrahim Juma ameiomba Serikali kuajiri watumishi zaidi wa idara ya mahakama ili waweze kufanya kazi katika mahakama mbalimbali zinazoanzishwa hapa nchini na hivyo kutoa haki kwa wakati kwa wananchi.
Kaulimbiu ya siku ya mahakama kwa mwaka huu ni Uwekezaji na Biashara: Wajibu wa Mahakama na Wadau kuweka Mazingira Wezeshi ya Uwekezaji.