Huzuni yatawala anayedaiwa kumuua dada yake Moshi

0
753

Kijana Leon Lazaro wa Kijiji cha Singa, Kibosho wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro amekuwa tishio katika kijiji hicho baada ya kudaiwa kufanya matukio mengi ya kiuhalifu ikiwemo wizi wa ng’ombe na mauaji ya dada yake Magreth Mushi.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Singa Kati anapoishi kijana huyo, Pantaleo Robert amesema mtuhumiwa amefanya tukio la kumkata mkono Anna Massawe ambaye ni mfanyakazi wa Hospitali ya Kibosho pamoja na kuiba ng’ombe katika nyumba mbalimbali kwenye kitongoji hicho.

Amesema mara baada ya kutekeleza tukio la mauaji ya dada yake, kijana Leon alikimbilia kwa ndugu yake mwingine na ndipo walipofanikiwa kumkamata kwa kushirikiana na jeshi la polisi.

Mwenyekiti huyo wa kitongoji amesema hali hiyo imechangia wananchi kumkimbia pindi wanapobaini uwepo wa kijana huyo kijijini hapo.

Kwa upande wake mama mzazi wa mtuhumiwa, Juliana Lazaro amesema kijana wake alikuwa mjeuri licha ya kumuonya mara kwa mara, na amekuwa akimtishia kutaka kumuua.

Kaka wa mtuhumiwa huyo, Aloyce Lazaro ameiomba serikali kuingilia kati suala la mdogo wake kwani iwapo ataachiwa ataendelea kufanya mauaji katika familia yao.

Kwa upande wake Kaimu kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro, Ronald Makona amesema tayari wameshamkamata mtuhumiwa na upelelezi unaendelea ili afikishwe mahakamani.