Huduma ya kujipima VVU mahala pa kazi yaanza

0
164

Serikali kupitia Wizara ya Afya imeanzisha huduma ya kujipima Virusi vya Ukimwi (VVU) mahala pa kazi ili kurahisisha upatikanaji wa huduma hiyo kwa watumishi makazini hasa wanaume, ambapo hadi kufikia Desemba 2022 watu wapatao 96,231 wamepatiwa huduma ya jipime mahala pa kazi.

Hayo yamejiri leo Januari 13, 2023, jijini Dodoma wakati wakati Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel akiwasilisha taarifa kuhusu kuhuisha na kujumuisha masuala ya UKIMWI mbele ya kamati ya kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI.

“Wizara imeanzisha huduma ya kujipima VVU (jipime) mahala pa kazi ili kurahisisha upatikanaji wa huduma ya vipimo vya VVU kwa watumishi sehemu za kazi hususani wanaume,” amesema.

Sambamba na hilo amesema, hadi kufikia Desemba 2022 jumla ya vijana balehe 47,705 (Wavulana 20,329 na Wasichana 27,376) walifikiwa katika shule zipatazo 103 kupitia kampeni ya Kipepeo, huku akibainisha kuwa, kampeni hiyo inatarajiwa kufanyika mwaka 2023 katika mikoa ya Dodoma, Singida, Morogoro, Tanga na Geita.