Historia ya mabadiliko ya mitaala ya elimu Tanzania

0
343

Mabadiliko ya jamii nchini Tanzania, kwa nyakati tofauti yamelazimisha mfumo wa utoaji elimu nchini kubadilika kuendana na matakwa ya wakati huo.

Mwaka 2021, Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeanza mchakato wa kufanya mabadiliko ya mitaala ya elimu katika ngazi za elimu za awali, msingi na sekondari, ili kuweza kupata wahitimu wenye ujuzi na maarifa yatakayokuwa na tija kwa wakati huu na ujao.

Mabadiliko haya ya sasa yatakuwa ni ya sita, lakini pengine hufahamu mabadiliko ya nyuma yalifanyika mwaka gani na yalikuwa na lengo gani. Tuangazie kwa ufupi mabadiliko hayo matano yaliyopita.

Mabadiliko ya kwanza yalifanyika mwaka 1967 ikiwa ni miaka sita tangu uhuru. Mabadiliko hayo yalilenga kuondoka mitaala ya kibaguzi iliyoanzishwa na wakoloni. Lengo lingine lilikuwa ni kujenga uzalendo kwa kuzingatia falsafa ya ujamaa ambapo vita ilikuwa dhidi ya maadui watatu ambao ni ujinga, maradhi na umasikini.

Baada ya miaka 12, Serikali iliona haja ya kufanya mabadiliko kwa mara ya pili, mabadiliko yaliyofanyika mwaka 1979. Msisitizo mkubwa kwenye mabadiliko haya ulikuwa kwenye elimu ya nadharia na vitendo na kupelekea kuanzishwa kwa michepuo ya masomo ya kilimo, ufundi na sayansi kimu.

Miaka 18 baadaye, Serikali iliamua kurudi tena mezani mwaka 1997 na kufanya mabadiliko mengine kwa kuzingatia pamoja na mambo mengine matakwa ya sera ya elimu ya mwaka 1995. Msisitizo ulikuwa katika kuboresha utoaji wa elimu kwa vitendo, ili kuwezesha, hasa vijana kujikwamu kiuchumi, kujengewa ari na uzalendo, ukiwa ni mwendelezo wa kile kilichoanzishwa mwaka 1967.

Mara ya nne mabadiliko kufanyika kwenye mitaala ya elimu ilikuwa mwaka 2005 ambapo hapa Serikali iliweka msisitizo kwenye ufunzaji na ujifunzaji umahiri (competency based carriculum), Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), uchopekaji wa elimu ya UKIMWI, afya ya uzazi, stadi za maisha na mazingira ambapo haya yalikusudia kukidhi mabadiliko ya jamii.

Mabadiliko ya mwisho yalikuwa mwaka 2014 ambapo mkazo ulikuwa kuboresha ufundishaji katika elimu ya awali na msingi. Msisitizo ulikuwa ni kujenga ujuzi, kuimarisha stadi za kuandika, kuhesabu na kusoma. Katika hatua hii, Wanafunzi wa darasa la kwanza na la pili walitakiwa kusoma masomo mawili tu, kusoma na kuhesabu.

Wanafunzi wa kwanza kuanza kutumia mtaala wa mwaka 2014 ndio wanatarajiwa kufanya mtihani wa kuhitimu darasa wa saba mwaka huu wa 2021.