Historia: MOI yafanya uchunguzi wa mishipa ya ubongo bila kufungua fuvu la kichwa

0
252

Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) imeandika historia ambapo kwa mara ya kwanza imeanza kutoa huduma ya uchunguzi wa mishipa ya damu kwenye ubongo, bila kufungua fuvu la kichwa katika maabara ya kisasa ya upasuaji wa ubongo (Angio Suite).

Uchunguzi huo umefanywa kwa saa 3 na jopo la madaktari bingwa, wauguzi, watalamu wa radiolojia sita kutoka MOI, Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) pamoja na hospitali ya Aga khan.

Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dkt. Respicious Boniface amesema kuanza kwa maabara hiyo ni ishara ya mageuzi makubwa katika sekta ya afya hapa nchini kwani maabara ya kisasa kama hiyo haipo kwenye nchi nyingine kwenye ukanda wa afrika mashariki kati.

“Leo ni siku ya furaha sana kwani tumeanza kutumia maabara yetu ya upasuaji wa ubongo (Angio suite), hii imewezekana kutokana na dhamira ya dhati ya Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli ya kuboresha huduma za afya hapa nchini kwani maabara hii imejengwa Serikali ya awamu ya tano kwa zaidi ya shilingi bilioni 7.9, kwa kweli tunamshukuru sana Mhe. Rais,” amesema Dkt. Boniface.

Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Ubongo MOI, Lemery Mchome amesema kuanza kwa maabara hiyo kumeleta mageuzi makubwa katika huduma za uchunguzi na upasuaji wa ubongo hapa nchini kwani hakuna mgonjwa atakayelazimika kwenda nje ya nchi kufuata huduma hii ambayo ilikuwa haipatikani hapa nchini.

“Tunashukuru upasuaji umefanyika salama na kwa mafanikio makubwa, tumeweza kufika kwenye ubongo wa mgonjwa bila kufungua fuvu, tumefanya upasuaji huu katika mazingizra mazuri kwani mitambo hii ni ya kisasa sana, kama mnavyoona mgonjwa yuko macho na anaongea vizuri kabisa ,hana kovu wala maumivu, hii ni hatua kubwa sana kwetu kama wataalamu,” amesema.

Mgonjwa aliyefanyiwa upasuaji huo, Hafidhi Said kutoka mkoani Singida amemshukuru Mungu kwa huduma aliyopata kwani amekuwa akipata maumivu kwa kipindi kirefu bila kujua anasumbuliwa na ugonjwa gani.