Heri ya miaka 57 ya Muungano

0
366

Watanzania leo wanaadhimisha miaka 57 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Kauli mbiu ya maadhimisho hayo kwa mwaka huu ni , Muungano Wetu ni Msingi Imara wa Mapinduzi ya Kiuchumi, Tudumishe Mshikamano Wetu.

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliundwa Aprili 26 mwaka 1964 ikiwa ni Muungano wa mataifa mawili huru ya Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, ambayo yaliingia mkataba wa Muungano
mwaka 1964 na kuanzishwa dola ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mkataba wa Muungano ulitiwa saini na aliyekuwa Rais wa Tanganyika, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Hayati Sheikh Abeid Amani Karume Aprili 22 mwaka 1964 huko Zanzibar.

Mkataba huo ulithibitishwa na Bunge la Tanganyika na Baraza la Mapinduzi Zanzibar tarehe 26 Aprili mwaka 1964.

Tarehe 27 Aprili mwaka 1964, viongozi wa nchi zote mbili walikutana katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es salaam na kubadilishana hati za Muungano.

Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliasisiwa kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa mahusiano ya karibu na ya kihistoria baina ya Tanganyika na Zanzibar katika nyanja mbalimbali kama vile udugu wa damu, biashara, utamaduni, lugha na mahusiano ya karibu kisiasa hasa baina ya vyama vya TANU na ASP.