Hedhi Salama, Afya Salama

0
378

Leo Mei 28 ni Siku ya Hedhi Salama Duniani (Menstrual Hygiene Day) ambapo huadhimishwa kwa lengo la kuhimiza umuhimu wa hedhi salama kwa Wasichana/Wanawake.

Siku hii ilianzishwa na Shirika lisilo la Kiserikali la Ujerumani (Wash United) mwaka 2014.

Licha ya juhudi nyingi za serikali, mashirika ya kijamii na watu binafsi kumsitiri mtoto wa kike na mwanamke kwa kuhakikisha anapata hedhi iliyo salama, bado kuna changamoto nyingi.

Baadhi ya changamoto zinazowakabili ni pamoja na elimu duni kuhusu suala la hedhi, gharama ya taulo za kike, upatikanaji wa taulo hizo, mazingira safi ya kubadili taulo hizo na mila za jamii mbalimbali.

Kutokana na changamoto hizo, baadhi ya watoto wa kike wamekuwa wakishindwa kuhudhuria masomo kwa kipindi chote cha hedhi kila mwezi, na hivyo kuwa kikwazo katika maendeleo yao kitaaluma.

Hiyo ni moja ya sababu zinazokwamisha lengo namba 5 la malengo ya maendeleo endelevu, SDG kuhusu usawa wa kijinsia.

Kutatua changamoto hizo inahitaji nguvu ya pamoja ya jamii yote (bila kujali jinsia), kwani hedhi inamhusu pia Mwanaume.