Hatutaki wanyama waingie kwenye makazi ya watu

0
118

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema serikali inaendelea kuimarisha mifumo itakayozuia wanyamapori wakiwemo tembo kuingia katika makazi ya watu.
 
Amesema baada ya serikali kuimarisha ulinzi na kuzuia uwindaji haramu, kwa sasa kuna ongezeko kubwa la wanyama nchini, hivyo jitihada zinafanyika kuzuia wanyama hao kuingia katika makazi ya watu.
 
Waziri Mkuu ameyasema hayo bungeni jijini Dodoma wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu ambapo mbunge wa jimbo.la Mlalo mkoani Tanga, Rashidi Shangazi alihoji ni kwa kiasi gani serikali inawahakikishia wananchi wanaoishi pembezoni mwa hifadhi usalama wao ili wasiendelee kupata athari kutokana na uvamizi wa wanyama hao.
 
“Serikali ina wajibu wa kulinda mali na usalama wa raia ndani ya nchi, tayari  tumeongeza idadi ya askari wa wanyamapori ambao tunawapeleka kwenye mbuga zilizo karibu na makazi ya watu.” ameongeza Waziri Mkuu Majaliwa
 
Amesema jitihada nyingine ni pamoja na kuimarisha na kujenga vituo vya kuhifadhi silaha ili kusaidia kuwaondoa wanyama hao na kuwarudisha katika maeneo yao ya hifadhi.