Hatukufanya maadhimisho ya miaka 57 ya Muungano kutokana na kifo cha Dkt. Magufuli

0
190

Hatukufanya maadhimisho ya miaka 57 ya Muungano kutokana na kifo cha Dkt. Magufuli

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango amesema Serikali iliamua kutokufanya sherehe za Muungano wa Tanzania mwaka huu kwa sababu ya kuondokewa na aliyekuwa Rais wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli Machi 17 mwaka huu.

Akizungumza katika Kongamano la Muungano, leo April 26, 2021 Chimwaga mkoani Dodoma, Dkt. Mpango amesema fedha zilizotengwa kwa sherehe hizo zitagawanywa kwa Serikali za Tanzania Bara na Zanzibar.

“Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni tunu na urithi mkubwa wa Taifa letu na hatuna budi kuendelea kuulinda, kuutunza, kuuenzi  na kuelimisha umma kuhusu umuhimu wake,” amesema Dkt. Mpango

“Baada ya nchi yetu kuondokewa na mmoja wa mashujaa wake, Dkt. John Pombe Magufuli, tuliamua  badala ya sherehe tuadhimishe muungano wetu adhimu kwa kuwa na kongamano hili.”

“Kwa busara za mama yetu Samia Suluhu Hassan ameagiza fedha zilizokuwa zitumike kwa ajili ya sherehe za muungano mwaka huu, zitagawanywa kwenda pande zote mbili za muungano kwa ajili ya shughuli za maendeleo,”  ameongeza Dkt. Mpango.

Kauli mbiu ya maadhimisho hayo kwa mwaka huu 2021 ni “Muungano Wetu ni Msingi Imara wa Mapinduzi ya Kiuchumi, Tudumishe Mshikamano Wetu”

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliundwa Aprili 26 mwaka 1964 ikiwa ni Muungano wa mataifa mawili huru ya Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, ambayo yaliingia mkataba wa Muungano mwaka 1964 na kuanzishwa dola ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.