Halmashauri zaagizwa kujenga matundu ya vyoo mashuleni

0
176

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Ummy Mwalimu amewaagiza Wakurugenzi wa halmashauri zote nchini kutumia mapato ya ndani kujenga matundu ya vyoo katika shule mbalimbali kabla wanafunzi hawajaripoti tarehe 17 mwezi huu.

Waziri Ummy ametoa kauli hiyo jijini Tanga wakati akikagua ujenzi wa vyumba vya madarasa kwenye shule mpya iliyojengwa katika eneo la Saruji.

“Madarasa tumekamilisha vizuri sasa naomba kutoa agizo kwa Wakurugenzi wote nchini kutumia fedha za mapato yao ya ndani kujenga vyoo, na hili lifanyike mapema iwezekanavyo kabla watoto wetu kurejea mashuleni.” ameagiza Waziri Ummy Mwalimu

Ameelekeza kuwa kila chumba cha darasa kinapaswa kuwa na matundu mawili ya vyoo.

Waziri huyo wa TAMISEMI pia amewaagiza Viongozi wa ngazi za vijiji, mitaa, kata na wilaya kushirikiana ili kuhakikisha watoto wote waliofikia umri wa kwenda shule kwenye maeneo yao wanaandikishwa na kuanza masomo kwa wakati.