Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imewaomba wafanyabiashara ndogondogo maarufu kama machinga walioweka vibanda vya kudumu katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo kuviondoa na badala yake wanatakiwa kutumia meza zenye maumbo yanayohamishika.
Afisa uhusiano wa Manispaa hiyo Tabu Shaibu amesema Halmashauri ya Jiji haijazuia wafanyabiashara ndogondogo kufanya biashara zao bali wanatakiwa kutumia meza ili kuondoa usumbufu ambao umekuwa ukijitokeza kwa watumiaji wa barabara.
Afisa Habari huyo ameelezea kuwa agizo la kuondoa vibanda hivyo ifikapo Mei 18 mwaka huu linasogezwa mbele mapaka mwisho wa mwezi huu.
Tabu ameongeza kuwa, Jiji linatambua umuhimu wa wafanyabiashara ndogondogo na hivyo inachofanya ni kuboresha maeneo yao ya kufanyia biashara na kuwawezesha wenye maduka kufanya shughuli zao
Hivi karibuni Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam lilitoa tangazo la kuwataka wafanyabiashara kuondoa vibanda vyao na kutumia meza zenye maumbo yanayokubalika katika maeneo hayo.