HALI YA ULINZI NA USALAMA WA MIPAKA YA TANZANIA

0
779

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Stergomena Lawrence Tax amesema katika mwaka wa fedha wa 2021/2022, hali ya mipaka ya Tanzania yenye urefu wa jumla ya kilomita 5,461.20 inayohusisha eneo la nchi kavu na eneo la maji, imeendelea kuwa shwari.

Ameliambia bunge jijini Dodoma kuwa mipaka hiyo ni baina ya Tanzania na Msumbiji, Malawi, Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Burundi, Rwanda, Uganda na Kenya.

Amesema katika kipindi hicho hapakuwa na matukio ya uhasama yaliyoripotiwa baina ya Tanzania na nchi inazopakana nazo, licha ya kuwepo kwa changamoto kadhaa.

Dkt. Stergomena ameelezea hali ya ulinzi na usalama wa mipaka ya Tanzania na nchi inayopakana nazo ;

Mpaka wa Tanzania na Msumbiji

“Hali ya usalama wa mpaka huu ni ya wastani kutokana na mashambulizi yanayofanywa na kundi la kigaidi la Ansar Al Sunna Wal Jamaah (AASWJ) maeneo ya Kaskazini mwa Msumbiji, katika Jimbo la Cabo Delgado linalopakana na mkoa wa Mtwara. Kundi hilo limekuwa likiathiri usalama kwa kuharibu na kupora mali za wananchi. Katika kupambana na changamoto hii, JWTZ imeendelea kuimarisha ulinzi kwa kufanya operesheni za ndani ya nchi na kukabiliana na kundi hilo. Aidha, JWTZ inashiriki operesheni chini ya Mwamvuli wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika nchini Msumbiji (SADC Mission in Mozambique – SAMIM) katika jitihada za kudhibiti ugaidi. Operesheni hizi zimeendelea kuimarisha ulinzi katika eneo la Mpaka, kudumisha amani na utulivu.” Dkt. Stergomena Lawrence Tax

Amewahakikishia wabunge kuwa operesheni zimesaidia kupunguza nguvu ya kundi hilo la kigaidi. Hata hivyo, kundi hilo linatekeleza mashambulizi kwa kuhamahama na kubadili mbinu za kimapigano. Licha ya hali hiyo, vikundi vya Tanzania vinaendelea kupambana kuhakikisha kundi hilo halileti madhara.

Mpaka wa Tanzania na Malawi

“Hali ya usalama ya mpaka huu ni shwari. Hakuna tukio la kuhatarisha usalama lililoripotiwa. Ushirikiano uliopo baina ya Jeshi letu na Jeshi la Malawi ni mzuri. Hali hiyo inajidhihirisha kutokana na mahusiano mazuri 29 yaliyopo, ambayo yamepelekea kufanyika michezo ya kirafiki kati ya timu za majeshi ya nchi hizi mbili yaliyofanyika Brigedi ya Kusini mwezi Julai 2021.” amesema Dkt. Stergomena

Amesema changamoto ya mpaka katika Ziwa Nyasa inaendelea kufanyiwa kazi kupitia Tume Maalum ya Usuluhishi iliyoundwa na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na kwamba serikali kupitia wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inaendelea kutumia njia za kidiplomasia ili kulipatia ufumbuzi wa kudumu suala hilo.

Mpaka wa Tanzania na Zambia

“Hali ya usalama katika mpaka huu ni shwari. Hakuna tukio la kuhatarisha usalama wa nchi yetu lililoripotiwa hadi sasa.” Dkt. Stergomena Tax

Mpaka wa Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo

“Hali ya usalama wa mpaka huu ni shwari. Hakuna tukio la kuhatarisha usalama kwa nchi yetu. Hata hivyo, ndani ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo yameripotiwa matukio ya waasi kushambulia miji mbalimbali nchini humo. Wizara kupitia JWTZ imeendelea kuwa macho na kujipanga wakati wote.” Dkt. Stergomena Lawrence Tax

Mpaka wa Tanzania na Burundi

“Hali ya usalama wa mpaka huu ni shwari, hakuna matukio yoyote yaliyoripotiwa kuhatarisha usalama baina ya nchi hizi, ingawa eneo hili linakabiliwa na uwepo wa wahamiaji haramu, uvamizi wa wakulima na uingizaji wa mifugo kwa ajili ya kupata malisho. JWTZ imeendelea kukabiliana na hali hii.” Dkt. Stergomena Lawrence Tax

Mpaka wa Tanzania na Rwanda

“Hali ya usalama wa mpaka huu ni shwari, ingawa yapo matukio machache ya kihalifu ya wahamiaji haramu na uingizaji wa mifugo kwa ajili ya malisho. Wizara kupitia JWTZ inaendelea kuchukua hatua aàza kudhibiti matukio hayo.” Dkt. Stergomena Lawrence Tax

Mpaka wa Tanzania na Uganda

“Hali ya usalama katika mpaka huu ni shwari. Hakuna tukio la kuhatarisha usalama wa nchi yetu. Hata hivyo, kuna changamoto ya uingizaji haramu wa mifugo kwa ajili ya malisho. Juhudi za kuimarisha mpaka zinaendelea kwa kuongeza Beacon kati ya marundo ya mawe yaliyowekwa na mkoloni na kujenga barabara ya usalama kwenye Mpaka.” Dkt. Stergomena Lawrence Tax

Mpaka wa Tanzania na Kenya

“Hali ya usalama wa mpaka huu, ni shwari. Hakuna tukio la kuhatarisha usalama dhidi ya Tanzania lililoripotiwa. Hata hivyo, ipo changamoto ya kuharibiwa kwa alama za mpaka. Kazi ya kuimarisha Mpaka huu inayotekelezwa na timu ya wataalam kutoka Tanzania na Kenya inaendelea vizuri, ambapo awamu ya kwanza imeanzia eneo la Serengeti hadi Ziwa Natron.” Dkt. Stergomena Lawrence Tax

Mpaka wa Tanzania katika Bahari ya Hindi

“Hali ya usalama wa mpaka huu, ni shwari. Katika Mpaka huu tumepakana na nchi za Comoro na Shelisheli. Hakuna tukio lililoripotiwa la kuhatarisha usalama dhidi ya Tanzania. Aidha, JWTZ imeendelea kufanya doria za mara kwa mara katika eneo la Bahari ya Hindi ili kubaini na kuzuia wahamiaji haramu, usafirishaji haramu wa binadamu, usafirishaji wa dawa za kulevya na matishio ya kigaidi.” Dkt. Stergomena Lawrence Tax

Dkt. Stergomena Lawrence Tax ameyasema hayo wakati akiwasilisha bajeti ya wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023 ambapo tayari bunge limeijadili na kuipitisha bajeti hiyo.