Hakuna malalamiko ya Fidia EACOP

0
147

Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limesema
hakuna mwananchi yeyote aliyetoa malalamiko ya kutoridhishwa na zoezi la ulipaji fidia baada ya kutoa eneo lake kupisha mradi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki (EACOP).

Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano kutoka TPDC Marie Msellemu ameyasema hayo mkoani Dodoma, wakati wa mahojiano maalum na Redio Jamii ya TBC Dodoma.

Amesema shilingi milioni 62 zimelipwa kama fidia kwa kaya 15 kwenye maeneo ya kipaumbele, ili kupisha mradi kambi namba 12 ambapo utajengwa katika kijiji cha Serya wilayani kondoa.

Kwa mkoa wa Dodoma pekee, mradi wa
EACOP unapita katika wilaya mbili ambazo ni Chemba na Kondoa.

Msellemu amesema wasimamizi wa mradi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki wanaendelea kutoa elimu kwa wananchi, kuhusu fursa zinazopatikana kupitia mradi huo.

Aidha ametoa wito kwa wananchi hasa wa maeneo unapopita mradi huo kujisaji kwenye kanzi data ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), ili kutambulika na kushirikishwa katika fursa mbalimbali.

Bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki kutoka Hoima, Uganda hadi Chongoleani, Tanga lina urefu wa kilomita 1, 447 na linatarajiwa kuzalisha ajira zaidi ya elfu kumi.

Ujenzi wake utagharimu zaidi ya shilingi trilioni 11 hadi kukamilika kwake.

Bomba hilo lina urefu wa kilomita 1,447 huku Tanzania pekee ikiwa na kilomita 1,147.