Gereza la wilaya ya Ruangwa lafunguliwa

0
556

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameuagiza uongozi wa Jeshi la Magereza nchini, kukamilisha ujenzi wa magereza za wilaya kwa wilaya zisizokuwa na magereza hizo.

Waziri Mkuu Majaliwa ametoa agizo hilo mkoani Lindi, wakati akifungua gereza la wilaya ya Ruangwa  na kuongeza kuwa,  uwepo wa magereza katika wilaya zote nchini utasaidia kumaliza tatizo la msongamano wa wafungwa na mahabusu kwenye magereza ya jirani.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu Majaliwa,  ufunguzi wa gereza hilo la wilaya ya Ruangwa,  utaondoa tatizo la msongamano wa wafungwa na mahabusu katika gereza la wilaya ya Nachingwea. 

Awali wakazi wa wilaya ya Ruangwa waliokua wakikabiliwa na tuhuma mbalimbali au waliohukumiwa kutumikia kifungo gerezani,  walikuwa wakipelekwa katika gereza la wilaya ya Nachingwea, jambo ambalo lilikua likiwanyima fursa ya kuonana na ndugu au mawakili wao kutokana na umbali uliokuwepo.

Awali, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Kangi Lugola alimweleza Waziri Mkuu Majaliwa kuwa,  gereza hilo la wilaya ya Ruangwa ni  muhimu katika kuimarisha ulinzi na usalama wa wilaya hiyo.

 Amesema gereza hilo ni chachu ya kuimarika kwa uchumi wa wilaya hiyo kwa kupitia sekta ya kilimo,  kwani kutakuwa na kambi za kilimo zitakazotoa fursa kwa wananchi kujifunza.  

  “Wananchi msilione gereza hili kama adui kwenu, halijaja kuwafunga,  bali lipo kwa ajili ya kuimarisha amani, ulinzi na usalama wa wilaya yetu pamoja na kutoa elimu mbalimbali”, amesisitiza Waziri Lugola.

 Kwa upande wake Kamishna Jenerali wa Magereza, –  Phaustine Kasike amesema kuwa,  ujenzi wa gereza hilo la wilaya ya  Ruangwa umefanywa na kikosi cha ujenzi cha Magereza kwa kutumia nguvukazi ya wafungwa.

Amesema awamu ya kwanza ya ujenzi wa gereza hilo imekamilika kwa gharama ya Shilingi Bilioni Moja Nukta Tano,  na hivyo kukamilisha uwepo wa magereza katika wilaya zote za mkoa wa Lindi.

Kamishna Jenerali huyo wa Magereza amefafanua kuwa  ujenzi huo ungefanywa na mkandarasi wa nje,  ungegharimu Shilingi Bilioni 2.226 na kwa kutumia kikosi cha Magereza wameokoa Shilingi Milioni 635.675.

Kwa sasa gereza hilo  la wilaya ya Ruangwa lina uwezo wa kuhifadhi wahalifu kati ya 250 na 280 na likikamilika litakuwa na uwezo wa kuhifadhi wahalifu Mia Tano.