Fursa ya biashara katika nishati Jadidifu

0
197

Watanzania wameshauriwa kutumia fursa katika uzalishaji wa umeme wa kutumia nishati jadidifu na kuuza umeme huo kwenye Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) au kutoa huduma kwa Wananchi.
 
Akitoa taarifa ya miradi ya uzalishaji wa umeme kwa kutumia nishati jadidifu katika mafunzo kwa Waandishi wa habari yaliyoandaliwa na shirika lisilo la Kiserikali la Haki Madini huko mkoani Pwani,  Mhandisi Victor Labaa kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) amesema mamlaka hiyo imeweka mazingira mazuri kwa wanaotaka kuzalisha umeme kwa kutumia nishati jadidifu na kuuza TANESCO na hivyo  kuongeza kiwango cha umeme katika gridi ya Taifa.
 
Mhandisi Labaa amesema EWURA imeruhusu wazalishaji umeme chini ya Kilowati 100 kutokata leseni ili kuzalisha umeme, na wale wanaozalisha zaidi ya hapo vigezo vimewekwa wazi.
 
Baadhi ya miradi ambayo imekuwa ikizalisha umeme kwa kutumia nishati jadidifu ni Andoya , Mwenga, Matembwe, Yovi, Tulila, Darakuta, Luponde, TPC Ltd , Kigoma Solar, miradi ambayo imekuwa ikizalisha umeme wa jumla ya Megawati 26.6 ikifaidisha Wananchi wa  maeneo mbalimbali nchini hasa wa vijijini.
 
Kwa mujibu wa Mhandisi Labaa, pia kumekuwa na wazalishaji wadogo zaidi (VSPP) ambapo hadi kufikia mwezi Julai  mwaka huu walifikia 122 ambao wamekuwa wakizalisha umeme wa Kilowati 3 mpaka 70.