Filamu ya Royal Tour kuoneshwa kwa umma Mei 8

0
6411

Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Filamu ya Tanzania: The Royal Tour amesema kuwa filamu hiyo itaoneshwa kwa wananchi wote kupitia vituo vya televisheni vya ndani Mei 8 mwaka huu.

Dkt. Hassan Abbasi amesema kwamba wanatambua shauku kubwa ya wananchi kuona kazi iliyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan kutangaza uwekezaji na utalii nchini Tanzania.

Abbasi ambaye ni Katibu Mkuu wa wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo amesema kuna baadhi ya mambo yanakamilishwa ikiwemo kuweka nukuu za kiswahili, ili kuwezesha wananchi wote kuielewa.

Ameongeza kuwa, wakati filamu hiyo itakapozinduliwa jijini Dar es Salaam, itarushwa kwenye televisheni ikiwemo Tanzania Safari Channel na TBC1.

Filamu hiyo inatarajiwa kuvutia watalii wengi zaidi, kuleta wawekezaji ambavyo vyote kwa pamoja vitakuza pato la Taifa, ajira na kuendelea kuitangaza Tanzania.