Fedha za Uviko-19 zaboresha Hospitali ya Dodoma

0
107

Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma imetumia vyema kiasi cha shilingi bilioni 4.6 kilichotolewa kwao na serikali ikiwa ni sehemu ya bilioni 263 ya fedha za ahueni ya UVIKO-19 ili kuboresha hospitali za rufaa za mikoa.

Hospitali hiyo imejenga jengo la wagonjwa mahututi (ICU) litakalokuwa na uwezo wa kulaza wagonjwa 50 kwa wakati mmoja pamoja kutoka 18 na ununuzi wa vifaa tiba.

Hayo yamebainiashwa leo na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu wakati alipotembelea Hospitali hiyo kujionea utekelezwaji wa ujenzi huo ambapo mbali na jengo la ICU, kutajengwa pia jengo la Radiolojia (CT-Scan), nyumba ya mtumishi pamoja na ukarabati wa jengo la huduma za dharura (EMD).

“Fedha hizi tulizowezeshwa na Rais Samia Suluhu Hassan, sasa Wizara ya afya kipaumbele chetu ni ubora wa huduma, hivyo kutokana na vitanda hivyo tutaweza kuwahudumia wagonjwa mahututi 50 ikiwa ni utekelezaji wa maono na dhamira ya Mheshimiwa Rais,” amesema Waziri Ummy.

Aidha, Waziri Ummy amesema kwa jengo la Radiolojia ambalo litawekwa mashine ya CT-Scan ambapo huduma hiyo haikuweppo hapo awali na hivyo itaweza kupunguza mzigo kwa wakazi wa Dodoma ambao walikuwa wanaenda kupata vipimo hivyo kwenye hospitali ya Benjamini Mkapa.

“Hospitali hii kwa mwezi wanapata wagonjwa 75 hadi 100 ambao wanapaswa kufanyiwa kipimo cha CT-Scan, hivyo huduma hii itawawezesha wananchi kupata kwa bei rahisi na kuwaondolea usumbufu hadi hospitali ya kanda ya Benjamini Mkapa,” ameongeza Waziri Ummy.

Kwa upande wa ukarabati wa jengo la huduma za dharura (EMD), waziri huyo amesema huduma zote za dharura zitapatikana katika eneo moja hivyo serikali imeweza kuboresha huduma za wagonjwa dharura kwani kutokuwa na huduma hizo unaweza kupoteza maisha ya watu.

Naye, Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo Dkt. Ernest Ibenzi amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa maboresho makubwa ya miundombinu na vifaa tiba katika hospitali ya Mkoa wa Dodoma ambayo yameweza kuboresha huduma za afya.

Dkt. Ibenzi amesema majengo hayo yatasogeza huduma zaidi kwa wananchi na hivyo kuondoa mrundikano wa wagonjwa hospitalini hapo na kuahidi wataendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuimarisha huduma za afya.