Kwa muda mrefu sasa kumekuwa na mkanganyiko kwa watumiaji wa lugha ya Kiswahili kuhusu matumizi sahihi ya maneno mawili, kumbukumbu na kumbukizi.
Baadhi ya watu wamekuwa wakitumia maneno hayo kana kwamba yote yana maana sawa, kama vile kutumia kumbukizi sehemu ya kumbukumbu, au kinyume chake, jambo linaloashiria kuwa watu wengi hawajui muktadha ambao maneno haya yanapaswa kutumika.
Ukweli ni kwamba maneno haya yana maana tofauti, na hivyo yanapaswa kutumiwa sehemu husika na sio neno moja kuwa mbadala wa jingine. Tuangalie maana na mifano ya matumizi ya maneno haya:
Kwa mujibu wa kamusi ya Kiswahili iliyotayarishwa na Baraza la Kiswahili la Tanzania (BAKITA) ya mwaka 2015, neno Kumbukumbu lina maana mbili, ambapo moja ni, fikra ya kudumu akilini mwa binadamu, au jambo linalokumbusha tukio lililopita. Maana ya pili ni muhtasari wa mambo yaliyojadiliwa katika mkutano au kikao kwa ajili ya rejea ya baadaye.
Kwa upande mwingine, Kumbukizi ni maadhimisho au sherehe ya kukumbuka na/au kuenzi jambo au kitu fulani kilichofanywa na mtu enzi za uhai wake au kilichofanya na mtu zamani.
Baada ya kuona maana ya maneno hayo sasa ni wazi kila mmoja ataweza kutoa mfano. Ni sahihi kusema (a) Februari 27 ni kumbukizi ya Vita vya Majimaji, ila si sahihi kusema (b) Februari 27 ni kumbukumbu ya Vita vya Majimaji.
Wakati huo huo ni sahihi kusema (a) Hawa wanafunzi wana kumbukumbu ya michezo ya utotoni, ila si sahihi kusema (b) Hawa wanafunzi hawana kumbukizi ya michezo ya utotoni.
Tukutane tena juma lijalo kuendelea kujifunza na kuienzi lugha hii adhimu ya Kiswahili.