Juni 30, 1964 Bendera ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilianza kutumika rasmi, ikiwa ni ishara ya muungano kati ya mataifa mawili Tanganyika na visiwa vya Zanzibar.
Awali Bendera ya Tanganyika kuanzia mwaka 1961 hadi 1964 ilikuwa na rangi tatu zilizopangwa kwa usawa kwa mpangilio wa kijani, njano, nyeusi, njano, kijani (kutoka chini kwenda juu) bila rangi ya bluu.
Kwa kipindi hicho Bendera ya Zanzibar nayo ilikuwa na rangi tatu, kwenye mpangilio huohuo wa kijani, nyeusi na bluu (kutoka chini) bila rangi ya njano.
Miezi miwili baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar Aprili 26, 1964 Tanzania ili kutengeneza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Tanzania ikatengeneza bendera yenye rangi nne zilizopangwa sambamba ikiwa ni muunganiko wa rangi za bendera za sehemu zote mbili zinazounganika.
Maana ya Rangi za Bendera ya Tanzania
KIJANI Rangi ya kijani katika bendera huonesha uoto (mimea) unaopatikana Tanzania.
NJANO Rangi ya njano katika bendera huwakilisha madini yanayopatikana katika ardhi ya nchi hii.
NYEUSI Hii husimama kuwakilisha Watanzania wenye asili ya weusi kama anavyofahamika mtu mweusi.
BLUU Tanzania ni nchi iliyopo kando mwa Bahari ya Hindi huku ikiwa imezungukwa na maziwa makubwa mbalimbali. Bluu huwakilisha vyanzo vyote vya maji ndani ya Tanzania.