Stakabadhi za mashine za EFD kuboreshwa

0
186

Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) limekwishatengeneza viwango vya ubora wa karatasi za stakabadhi za mashine za EFD.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Hamad Chande bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Angelina Malembeka mbunge wa viti maalum, aliyetaka kufahamu serikali ina mpango gani wa kuboresha stakabadhi za mashine za EFD ili zisifutike baada ya muda mfupi.

Amesema kufutika kwa stakabadhi za mashine za EFD baada ya muda mfupi kunasababishwa na matumizi ya karatasi zenye ubora hafifu na kwamba karatasi zinazotakiwa kutumika ni zile zenye ubora (Thermal paper).

“Baada ya kubaini hilo TBS kwa kushirikiana na TRA imeshatengeneza viwango vya ubora wa karatasi hizo zinazotakiwa, na sasa wanaendelea na usimamizi kuhakikisha karatasi zote zinakidhi ubora unaotakiwa.” amesema Naibu Waziri Chande

Ameongeza kuwa TRA imeboresha mfumo wa usimamizi wa mashine za EFD kwa kuwezesha kupokea taarifa zote za kila risiti zinazotolewa na kuitunza katika ‘server’ zake, na hivyo kuwezesha nakala ya risiti hizo kuweza kupatikana wakati wowote inapohitajika.