Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) imesimamisha mikutano yake yote iliyokuwa imepangwa kufanyika kutokana na virusi vya corona kuzidi kusambaa kwa kasi katik nchi mbalimbali.
Katika barua yake kwenda kwa Katibu Mkuu wa EAC, Liberat Mfumumkeko, Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda ambaye ndiye Mwenyekiti wa Baraza la EAC, Vicent Biruta ameagiza kusimamishwa kwa mikutano yote ambayo inahusisha idadi kubwa ya watu, hadi hapo itakapoamuliwa vinginevyo.
Kutokana na uamuzi huo, miongoni mwa mikutano ambayo itaathirika ni pamoja na Mkutano wa 21 wa EAC uliokuwa umepangwa kufanyika mwezi huu, pamoja na Mkutano wa 40 wa Baraza la Mawaziri wa EAC uliokuwa unatarajiwa kufanyika Aprili 14.
Aidha, mbali na kusimamisha mikutano hiyo Biruta ameelekeza kuwa mikutano inayohusisha watu wachache ifanyike kwa njia ya video pale inapowezekana.
Kabla ya uamuzi huo tayari baadhi ya nchi wanachama wa jumuiya hiyo walishachukua tahadhari kwa kuzuia mikutano yote ya kimataifa ili kudhibiti kuenea kwa virusi vya corona ambayo hadi sasa vimesababisha vifo vya zaidi ya watu 4,900 duniani kote.