Rais Samia Suluhu Hassan ameieleza dunia dhamira thabiti ya Tanzania ya kutekeleza mkakati wa kitaifa wa Nishati Safi ya Kupikia wa miaka 10 aliouzindua hivi karibuni wenye lengo la kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2030.
Rais amesema hayo wakati akishiriki kwenye mkutano wa kwanza wa kimataifa kuhusu Nishati Safi ya Kupikia jijini Paris, Ufaransa ulioandaliwa na Shirika la Nishati Duniani (IEA).
“Pia, nimeongeza sauti yangu kwa jamii ya kimataifa na wadau wa sekta hii kuongeza nguvu kisera na kifedha na kuufanya mwaka 2024 kuwa Mwaka wa Nishati Safi,” amesema Rais Samia kupitia mitandao ya kijamii.
Amesema ushiriki wake kwenye mkutano huo ni heshima kubwa kwa nchi yetu kutokana na kutambulika kwa juhudi zinazifanywa katika eneo hilo kiasi cha kupata nafasi ya kushiriki mjadala wa kimataifa kuhusu nishati safi ya kupikia ambapo majawabu yake amesema yatawafaa watu bilioni 2.3 duniani kote wanaoishi na changamoto hiyo ya nishati, milioni 900 kati yao wakiwa katika Bara la Afrika.
“Mabadiliko katika kuleta matumizi ya nishati safi ya kupikia ni hatua kubwa katika maendeleo ya watu wetu na yataakisi hatua tunazopiga kiuchumi na kwenye ukombozi wa mwanamke kwani hii ni moja ya changamoto kubwa kwao,” amesema Rais Samia.