Akitoa ripoti ya fedha zilizotumika kununua vishkwambi Laki tatu vyenye thamani ya shilingi Bilioni 123.7 kutoka kwa wazabuni watatu kwa ajili ya Sensa ya Watu na Makazi iliyofanyika mwezi Agosti mwaka 2022, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Charles Kichere amesema, zipo dosari kadhaa alizozibaini kwenye manunuzi ya vishkwambi hivyo.
Dosari hizo ni pamoja na kuingiliana majukumu kati ya bodi na idara nyingine, Wajumbe wa bodi ya zabuni kupendekeza wazabuni wanne huku wawili kati yao wakishinda huku ikifahamika wazi kuwa sio kazi ya bodi ya zabuni kupendekeza wazabuni.
Amesema bodi ya zabuni ilibadili vigezo vya ubora bila kuwasiliana na idara tumizi na kuondoa vifaa vya kutunzia umeme.
Kichere ameongeza kuwa bodi ya zabuni ilitoa siku mbili kwa wazabuni kujibu nyaraka za zabuni badala ya siku 14 kama inavyotakiwa, huku idara ya ununuzi ikiachwa bila kushirikishwa.
CAG Kichere alikua akikabidhi kwa Rais Samia Suluhu Hassan taarifa ya Ofisi yake kwa mwaka wa fedha wa 2021/2023.