Dorothy Semu kukaimu nafasi ya Maalim Seif

0
162

Chama cha ACT-Wazalendo kimesema kuwa makamu wa mwenyekiti wa chama hicho (Bara), Dorothy Semu ana kaimu nafasi ya uenyekiti wa chama iliyoachwa na Hayati Maalim Seif Sharif Hamad.

Chama hicho kimesema uamuzi huo ni kwa mujibu wa ibara ya 84(3) na (4) ya katiba ya ACT- Wazalendo ya mwaka 2015 toleo la mwaka 2020 ambayo inasomeka;

“84(3): iwapo mwenyekiti wa chama hayupo kwa sababu yoyote ile basi makamu mwenyekiti anayetoka upande mwengine wa muungano tofauti na anaotoka mwenyekiti, na kama makamu mwenyekiti aliyetajwa kwanza naye hayupo, basi makamu mwenyekiti aliyebakia atakaimu nafasi ya uenyekiti.

Aidha, chama kimeeleza kuwa kwa kuzingatia ibara ya 84(4) ya katiba ya ACT- Wazalendo, Semu ataendelea kukaimu nafasi hiyo ndani ya kipindi kisichozidi 12 hadi pale mwenyekiti mpya atakapochaguliwa na mkutano mkuu maalumu wa taifa wa chama hicho.

Maalim Seif ambaye alifariki dunia Februari 17 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), alikokuwa akipatiwa matibabu, alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa chama hicho Machi 2020.