Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi amewashukuru wananchi wa Dodoma na watanzania wote kwa namna ambavyo wamefanikisha Tamasha la Serengeti Music Festival Dodoma lililofanyika Februari 06, 2021 Uwanja katika wa Jamhuri jijini humo.
Dkt Abbasi ametoa Shukrani hizo jijini Dar es Salaam ambapo amesema, wakati wananchi wanatimiza wito wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli wa kufanya kazi, Wizara yake inayo wajibu wa kuwapa burudani wananchi.
“Nawapongeza na kuwashukuru wadau wote waliofanikisha Tamasha la Serengeti Music Festival, tumefanya kazi kubwa na kuionesha Afrika na Dunia kwa ujumla kuwa Tanzania ya kipato cha kati ambayo ni ya kazi zaidi lakini pia burudani ndio sehemu yake”, amesema Dkt. Abbasi.
Dkt. Abbasi amewashukuru wanadodoma kwa jinsi walivyokuwa na ari ya kupata burudani licha ya kuloa na mvua iliyokuwa inanyesha siku hiyo,hali iliyolazimu wasanii kuendelea kutoa burudani kwa hadhira hiyo.
Aidha, Dkt Abbasi amewashukuru wasanii, wadhamini, viongozi wa Serikali, wabunge wakiongozwa na Naibu Spika, Tulia Akson, wafanyakazi wa Wizara yake, washereheshaji, madjs, serikali ya wanafunzi, wanafunzi pamoja na watanzania wote kwa ujumla kwa kufanikisha tamasha hilo.