Dkt. Kikwete akabidhiwa nyumba ya kuishi

0
546

Rais Samia Suluhu Hassan amemkabidhi nyumba ya kuishi Rais Mstaafu, Dkt. Jakaya Kikwete iliyojengwa katika Wilaya ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam.

Nyumba hiyo imejengwa na Serikali ya Tanzania kupitia Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) ikiwa ni utekelezaji wa kifungu namba 12 cha Sheria ya mafao ya hitimisho la kazi kwa viongozi wa siasa, sura ya 225 na marejeo ya mwaka 2020 ambayo pamoja na stahili zingine za matunzo ya viongozi wakuu wastaafu inaelekeza kuwa Rais anayestaafu anastahili kujengewa nyumba ya kuishi yenye hadhi ya Rais.

Akizungumza baada ya kukabidhi nyumba hiyo, Rais amempongeza Dkt. Kikwete kwa kupata makazi hayo na amemhakikishia kuwa Serikali itaendelea kumtunza yeye na viongozi wengine wastaafu kama inavyoelekezwa katika sheria.

Amebainisha kuwa Serikali itafanyia kazi uboreshaji wa sheria hiyo pamoja na kuhakikisha wajane/wagane wa viongozi wanatunzwa.