Dkt. Shoo : Msiogope kuhesabi

0
178

Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dkt. Fredrick Shoo amewatoa wasiwasi watanzania wanaoogopa kushiriki zoezi la sensa ya watu na makazi kwa sababu za kidini kwa kusema kuwa, kuhesabiwa ni jambo muhimu hata vitabu vya dini vimeandika.

Dkt. Shoo ameyasema hayo mjini Moshi mkoani Kilimanjaro, wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya zoezi hilo na kuongeza kuwa katika vitabu vya dini ikiwemo Biblia, Agano jipya na lile la kale zipo taarifa za watu kuhesabiwa.

“Watu wanaogopa jambo la sensa kwa sababu eti za kidini, labda tu tukumbushane wakati mwokozi wetu Yesu Kristo anazaliwa tunaambiwa baba yake Yusuf na Mama yake Mariam walifika katika mji wao wa kuzaliwa kwa ajili ya kuhesabiwa.”
amefafanua Dkt. Shoo

Amesema suala la kuhesabiwa si kinyume na mapenzi ya Mungu, hivyo hakuna hofu ya watanzania kuogopa zoezi hilo badala yake wanatakiwa kushiriki kikamilifu, ili kuisaidia serikali kujua mahitaji kwa kila kundi.

Mkuu huyo wa KKKT pia amewataka makarani wa sensa kufanya zoezi hilo kwa uaminifu na kuchukua taarifa kwa usahihi na sio kuwauliza watu maswali katika hali ya kuwaogopesha.