Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amesema Rais Samia Suluhu Hassan ni muumini namba moja wa maridhiano nchini na haishii tu katika kusema, bali anatekeleza kwa vitendo huku nia ikiwa ni kuhakikisha kunakuwa na umoja na amani nchini.
Dkt. Biteko amesema hayo leo wakati wa Misa Maalum ya Kutabaruku Kanisa Kuu la Kiinjili la Kilutheri Tanzania ( KKKT) Lukajange, Dayosisi ya Karagwe iliyofanyika wilayani Karagwe, Mkoa wa Kagera.
“Rais Dkt. Samia anasema kila mara kuwa hii nchi ni yetu sote, anatuasa mara nyingi kuwa wewe kama ni CCM mpende mpinzani, na mpinzani mpende CCM, tuungane pamoja tusukume nchi yetu mbele,” amesisitiza Dkt. Biteko.
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko ametaka viongozi mbalimbali nchini kufanya kazi na watu wanaowaunga mkono na wasiowaunga mkono kwani wajibu wao ni kuwahudumia wananchi wote.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, Abdulrahman Kinana amempongeza Askofu Benson Bagonza kwa uongozi mzuri katika Dayosisi ya Karagwe na ujenzi wa kanisa kuu jipya katika dayosisi hiyo.
Kwa upande wake, Askofu Bagonza amemshukuru Rais Samia kwa kusimamia suala la maridhiano kwa makundi yanayoonesha kukinzana huku akisema kuwa upatanisho huo anaousimamia una baraka za Mungu na amemtia moyo wa kuendelea kusimamia maridhiano kwani ni afya ya Taifa.
Dayosisi ya Karagwe ilizinduliwa mwaka 1979 ambapo ujenzi wa kanisa hilo kuu ulianza mwezi Februari 24, 2023 na kukamilika Novemba 2023 kwa gharama ya shilingi milioni 400.