Dkt. Rioba aacha maswali Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani

0
416

Kukua kwa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) pamoja na mambo mengine kumerahisisha mawasiliano na ushirikishanaji na upashanaji habari, ambapo sasa tukio linalotokea sehemu nyingine au nchi nyingine unaweza kulipata wakati huo huo.

Akitoa wasilisho katika Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani ambayo kwa upande wa Afrika imefanyika Tanzania kwa mara ya kwanza, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Dkt. Ayub Rioba Chacha amesema TEHAMA imewapa uwezo walaji wa habari kukusanya, kuchakata, kuchambua na kutoa habari, imekuwa sauti kwa waliokuwa hawana sauti na imeibua vipaji bila kupita kwenye vyombo vya habari vya asili (redio, TV na gazeti), kuweka uzania wa taarifa, kutoa fursa za kibiashara na elimu.

Licha ya mafanikio hayo kuchangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa sekta ya habari nchini na duniani, TEHAMA haijaacha kuwa na  athari kwenye masuala ya habari hasa namna mitandao ya kijamii imeufifisha mstari unaomtenganisha mwanachi wa kawaida na mwandishi wa habari.

Ametaja baadhi ya vitu vilivyokumbana na rungu la TEHAMA ni mila na desturi za Afrika ambazo zimenyongwa mchana kweupe huku mitindo ya maisha ya Magharibi ikipewa nafasi kwenye jamii. Umoja wa kitaifa, usalama wa Taifa havikusalimika kwenye uvamizi huo kutokana na vikundi vya watu wenye nia ovu kusambaza taarifa za kibaguzi au zenye kuvunja amani.

Athari nyingine ni kutwezwa kwa utu, makundi ya kigaidi kutumia mitandao ya kijamii kupata wafuasi na kutekeleza mashambulizi, uzambazaji wa taarifa za uongo ambao tofauti na zamani ambako kulisababishwa na ukosefu wa habari hivyo watu wakaamini uzushi, sasa hivi kunasababishwa na uwepo wa taarifa nyingi, hivyo mtu anashindwa kuchuja ipi ya kweli na ipi ya uongo.

Akihitimisha wasilisho lake ameacha maswali wa kwa waandishi wenzake akihoji, ni kwa namna gani wanafunzi katika vyuo watafunzwa kuweza kukabiliana na mabadiliko haya? Ni kwa namna gani inawezakana kuhakikisha uhuru wa vyombo vya habari? Wanawasilishaje habari katika mazingira ya sasa? Wanafanye habari ziwe za kuvutia zaidi? Wamejiandaaje na uwepo wa wanahabari maroboti?

Katika maadhimisho hayo ambayo kaulimbiu yake ni Uandishi wa Habari na Changamoto za Kidijiti, Dkt. Rioba ameacha swali la mwisho kuwa, “Bado tunaamini kuwa ni serikali pekee inayopaswa kufuatiliwa? Kwamba sisi kama vyombo vya habari ni waangalizi?”