Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Damasi Ndumbaro amesema Serikali haitamzuia mtu yeyote anayetaka kuondoka kwa hiari katika eneo la Ngorongoro kwenda kuishi popote nchini, na kuwataka wadau wengine kutowazuia wanaotaka kuondoka katika eneo hilo.
Dkt. Ndumbaro ameyasema hayo mkoani Dar es Salaam wakati akizungumza na Mabalozi mbalimbali wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini, wakuu wa mashirika ya kimataifa na Wadau wa maendeleo kuhusu mpango wa Serikali wa kutafuta suluhu ya kudumu katika eneo la Ngorongoro na Loliondo.
Ameongeza kuwa Serikali itawawezesha wale wote wanaotaka kuondoka kwa hiari katika maeneo hayo.
Kwa mujibu wa Dkt. Ndumbaro, mpaka sasa jumla ya kaya 164 zenye watu 915 zimejiandikisha kuondoka Ngorongoro kwa hiari na kwenda kuishi katika maeneo mbadala watakayopewa na Serikali, ikiwa ni pamoja na kuwajengea nyumba ama kuwalipa fidia.
Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula amesema dhumuni la kuwaita Mabalozi hao wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini pamoja na wakuu wa Mashirika ya Kimataifa ni miongoni mwa jitihada zinazofanywa na Serikali kuhakikisha Mabalozi na wadau wa maendeleo wanapata taarifa sahihi kuhusu suala la Ngorongoro na Loliondo kutokana na suala hilo kugubikwa na upotoshaji.
Akichangia mjadala huo, Balozi wa Ujerumani nchini Regina Hess ameunga mkono jitihada za Serikali za kulinda uhifadhi na mazingira katika eneo la Ngorongoro ili kukabiliana na athari zinazotokana na mabadiliko ya tabia nchi.