Dkt. Ndumbaro afanya ukaguzi katika Mpaka wa Tanzania na Msumbiji (Ruvuma)

0
468

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro amefanya ziara katika eneo la Mpaka wa Mkenda uliopo Wilaya ya Songea Vijijini mkoani Ruvuma unaoinguanisha Tanzania na Msumbiji ili kibaini na kutatua changamoto mbalimbali na ili kukuza biashara na uhusiano wa kidiplomasia baina ya nchi hizo mbili.

Akiwa mpakani hapo Dkt. Ndumbaro amesikiliza changamoto na mapendekezo yanayolenga kuboresha namna ya utoaji huduma kwa wakazi wa eneo la mpaka na watumiaji wa mpaka huo, pamoja na kutoa ufumbuzi wa baadhi ya changamoto, na kuahidi kuzifanyia kazi changamoto zilizosalia.

Dkt. Ndumbaro pia ametembelea Ofisi za mpakani kwa upande wa Nchi jirani ya Msumbiji na kufanya mazungumzo na Watumishi walipo katika Ofisi hizo.

Ndumbaro ameeleza kuwa serikali inaendelea kutatua changamoto mbalimbali mpakani hapo ikiwemo ukosefu wa umeme, huduma ya mawasiliano na barabara ya kiwango cha lami na ujenzi wa Kituo cha Kutoa Huduma kwa Pamoja Mpakani (OSBP).

Dkt. Ndumbaro amewapongeza Watumishi walipo mpakani kwa kazi nzuri wanayoifanya na amewahimiza Watumishi hao kuendelea kutekeleza dilomasia ya Uchumi, kuendeleza uhusiano mwema na kushughulikia suala la diaspora.

Katika ziara hiyo Dkt. Ndumbaro aliambatana na Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi ya Wilaya ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Songea Vijijini, Pololet Mgema.