Dkt Mwinyi asisitiza Zanzibar kutangazwa Kimataifa

0
203

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Hussein Mwinyi amesema Zanzibar imeamua kujiimarisha katika sekta ya biashara na uwekezaji, hivyo Mabalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania popote walipo wana dhima ya kuitangaza vyema Zanzibar.

Dkt Mwinyi ameyasema hayo wakati wa mazungumzo yake na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Profesa Palamagamba Kabudi Ikulu jijini Zanzibar.

Rais Mwinyi amesema Mabalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni vema wakaitangaza Zanzibar katika Balozi zao nje ya nchi pamoja na kuangalia uwezekano wa kuitangaza sekta ya utalii na masoko hasa kwa bidhaa za viungo.

Amesema Mabalozi wana kila sababu ya kuitumia fursa hiyo kuitangaza Zanzibar nje ya nchi hasa ikizingatiwa kwamba Zanzibar ina vivutio vingi kwenye sekta ya utalii, masoko pamoja na mazingira mazuri ya uwekezaji.

Rais Dkt Mwinyi amesema wakati Mabalozi hao wakifanya kazi hiyo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kujenga uwezo katika kuimarisha uchumi wake.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Profesa Palamagamba Kabudi  amempongeza Rais Mwinyi kwa ushindi mkubwa alioupata katika uchaguzi mkuu uliopita.

Amesema ushindi huo unadhihirisha imani waliyonayo Wananchi wa Zanzibar kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais Mwinyi kufuatia ahadi alizozitoa wakati wa kampeni za uchaguzi hasa ile ya  kuimarisha uchumi, Muungano, umoja, mshikamano na maridhiano.