DKT. MWINYI ASISITIZA USHIRIKIANO NA UTURUKI

0
227

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Mwinyi amemtaka Balozi wa Tanzania nchini Uturuki, Idd Seif Bakari kuendeleza uhusiano uliopo, kudumisha Diplomasia ya kiuchumi, kusaidia kutafuta fursa mbalimbali za uwekezaji pamoja na biashara zinazopatikana nchi humo.

Dkt. Mwinyi ameyasema hayo alipokutana na Balozi Idd Seif Bakari aliyefika Ikulu Zanzibar kumuaga kuelekea katika kituo chake cha uwakilishi nchini Uturuki.

Aidha, Dkt. Mwinyi amegusia mambo matatu katika kufungua fursa za uwekezaji na biashara kati ya Zanzibar na Uturuki ikiwemo kupata wawekezaji katika viwanda, kuzitangaza fursa zilizopo katika sekta ya utalii wa fukwe za bahari na urithi pamoja na kujifunza na kutafuta fursa za uwekezaji zitokanazo na sekta ya miundombinu ikiwemo bandari, barabara na viwanja vya ndege.

Balozi Idd Seif Bakari aliteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa Balozi wa Tanzania nchini Uturuki Aprili 05, 2023 ambapo kabla ya uteuzi huo alikuwa Konseli Mkuu, Dubai.